Friday, August 13, 2010

Wali wa hoho


Wali wa hoho ni chakula maalum kinachotumika katika hafla au sherehe. Ni chakula chenye ladha nzuri na kina muonekano wa kuvutia kinapokuwa mezani tayari kwa kuliwa.

Mara nyingi huandaliwa kama zawadi katika harusi hususan kwa watu wa pwani. Kwa kuwa zawadi hiyo au maarufu kama kombe huwa kuna vyakula vingi, ikiwamo chakula hiki ambacho hufanya kombe kuwa na muonekano wa kupendeza.

Mbali na kuliwa kama kombe chakula hiki kinaweza kuandaliwa kama mlo wa usiku.

Mahitaji:
• Mchele ½ kg
• Nyanya 3
• Mafuta ya kupika ¼ kikombe cha chai
• Chumvi kiasi
• Kitunguu swaumu kilichosagwa kijiko 1 cha mezani
• Kitunguu maji kilichosagwa kijiko 1 cha mezani
• Hoho 4
• Nyama ya kusaga ¼
• Tangawizi kijiko 1 cha chakula
• Limao au ndimu kipande



Maadalizi:
• Chukua mchele uoshe vizuri kasha chuja maji
• Chukua nyama ya kusaga na kamulia ndimu, weka chumvi na tangawizi, changanya vizuri na weka jikoni.iache ichemke hadi ikauke maji yote.
• Chukua maji na kiasi cha robo tatu lita chemsha na weka pembeni
• Chukua sufuria kavu yenye uwezo wa kupika kiasi cha kilo moja
• Weka mafuta ya kupika kiasi cha vijiko vitatu na acha yapate moto
• Weka vitunguu maji, menya nyanya na katakata halafu weeka katika sufuria hiyo.
• Weka chumvi na kanga hadi vilainike kabisa
• Baada ya kuiva weka vitunguu swaumu na baadaye mchele
• Koroga hadi uchanganyike na weka nyama. Endelea kukoroga, baada ya hapo weka maji kiasi cha kuivisha mchele huo. Acha vichemke hadi vikaukie.
• Palia mkaa juu yake au kama unatumia jiko la gesi au umeme weka kwenye oven hadi maji yakauke kabisa.
• Baada ya hapo chukua hoho na kasha kata upande wa juu kama vifuniko. Kasha ondoa matunda ya ndani yake. Funika na kasha zipange kwenye sufuria yenye maji na chumvi na mafuta kidogo kiasi cha kijiko kimoja. Chemsha jikoni hadi ziive.
• Baada ya kuiva, chukua hoho zako na kasha chota wali kw akutumia kijiko kasha jaza katika kila hoho na weka kwenye sahani tayari kwa kuliwa.
• Unaweza kupamba na salad ukipenda.

Thursday, August 12, 2010

Jinsi ya kupika kisamvu bila nazi


Kisamvu ni aina ya mboga ya majani inayopatikana kwa wingi na kwa urahisi katika mikoa takriban yote nchini Tanzania.
Pia aina hii ya mboga hupikwa katika mapishi ya aina mbalimbali kulingana na mahitaji ya mpishi.

Aina hii ya mboga kama zilivyo mboga zingine za majani ni nzuri na muhimu kwa afya ya binadamu. Aina hii ya mboga huleta virutubisho mbalimbali mwilini.
Hapa tunaenda kuona mapishi ya kisamvu kwa kutumia mafuta bila nazi kama ilivyozoeleka na wengi.

Mahitaji :
• Kisamvu kilichotwangwa na kuwa laini
• Kitunguu maji
• Kitunguu swaumu
• Kunde mbichi
• carrots
• Mafuta ya kula
• Chumvi kiasi

Maandalizi :
• Chemsha kisamvu ukiwa umechanganya na kunde mpaka uhakikishe vyote vimeiva. Baada ya kuiva weak pembeni.
• Chukua sufuria kavu, weak mafuta kasha weak katika jiko na yakipata moto weak kitunguu na koroga mpaka kibadilike rangi kasha weak kitunguu swaumu na endelea kukoroga kwa muda baada ya hapo weak carrots na kisha weka kisamvu chako ambacho kimechanganywana kunde.
• Endelea kukoroga kwa muda na kasha acha kichemke mpaka uhakikishe mboga yako imeiva vizuri.
• Mboga hii iko tayari kwa kulikwa na inaweza ikaliwa na wali au ugali.

Mapishi ya Chicken Curry


Leo wapendwa nitaenda kuzungumzia mapishi ya mchuzi wa kuku (chicken curry).

Mahitaji
Kuku mzima
Nyanya kubwa 3
Karoti mbili
Pilipili hoho
Kotmiri
Tangawizi
Kitunguu maji
Kitunguu saumu kidogo
Ndimu
Mafuta ya kupikia
Chumvi (pilipili ukipenda)

Matayarisho
1. Menya vitunguu saumu na tangawizi na uvitwange pamoja.
2. Katakata kuku vipande vidogo kisha ukamulie ndimu na kupaka mchanganyiko wa tangawizi na vitunguu saumu (kiasi tu).
3. Katakata vitunguu maji na pilipili hoho uweke pembeni.
4. Grind (Kwangua) kwenye grater nyanya na karoti pia uweke pembeni.
5.Katakata kotmiri vipande vidogo uweke pembeni.
6. Andaa kikaango na jiko.

Mapishi
1. Bandika kikaango jikoni na mafuta kiasi, yakishachemka weka vitunguu maji na kaanga hadi vimelainika na kuiva (hakikisha haviungui).
2. Weka pilipili hoho na karoti na endelea kukoroga hadi vyote viive na kulainika, Kisha weka chumvi.
3. Sasa weka vipande vya nyama koroga na funikia kwa dakika 3, kisha weka nyanya zako ulizo grind na koroga ili zichanganyike vizuri, vikishachanganyika weka kotmiri na pilipili kama utapenda. Acha vichemke kwa dakika 5. Hakikisha moto sio mkali sana.
4. Angalia kama nyama zimeiva vizuri kisha epua mchuzi wako.
5. Pakua kwenye bakuli na katakata kotmiri uweke kwa juu.
Unaweza kula kwa ugali, wali, ndizi rost au chipsi.

Enjoy!

Mapishi – Fish Finger


Leo tunaangalia mapishi ya fish finger ( sijui kama unaweza kusema kidole cha samaki)!, Ni mlo mzuri hasa kuliwa kama kitafunio au mboga ya pembeni.

Mahitaji
500g Fileti ya samaki
120g Chenga za mkate
100g Unga wa ngano
Mayai 2
Ndimu 1
Kitunguu saumu 1
Kotmiri
Mafuta ya kupikia

Matayarisho
Menya vitunguu saumu kisha visage

Katakata fileti kwa muundo wa mraba (kama vidole) kisha paka mchanganyiko wa vitunguu saumu

Kata ndimu na kamulia kwenye fillet yako

Weka chenga za mkate kwenye bakuli kisha uchanganye chumvi kiasi na kata kata kotmiri majani 3 na uchanganye pamoja.

Kwenye bakuli lingine weka mayai na uyapigepige yawe kama uji mzito

Weka unga kwenye bakuli jingine.

Chukua kipande cha fillet kiweke unga kidogo kisha kizamishe kwenye yai na baada ya hapo kizamishe kwenye mchanganyiko wa chenga za mkate. Fanya hivyo kwa vipande vyote.

Weka mafuta kwenye kikaago na subiri yachemke kisha weka fillet zako vizuri na zikaange pande zote hadi zimekuwa rangi ya brown ( hakikisha moto sio mkali sana).

Epua na weka pembeni mafuta yote yakauke

Weka kwenye sahani tayari kwa kula.

Enjoy!

Mapishi – Mayai Mchanganyiko, Tosti na Soseji


Karibu tena jikoni, leo tunaandaa vitafunwa kwa ajili ya kifungua kinywa asubuhi.

Mahitaji
Mayai 3
Soseji 2
Mkate slesi 2
Mafuta ya kupikia vijiko 2
Chumvi

Matayarisho
Piga piga mayai vizuri kwenye bakuli na weka chumvi kidogo kisha weka kikaango kwenye moto na mafuta kidogo.

Kikisha pata moto miminia mchanganyiko wa mayai na uanze kukorogo pale tu unapomiminia, endelea kukoroga hadi uone yanakuwa magumu na kuanza kuiva. Pika kwa kiwango unachopendelea na kusha epua na weka kwenye sahani.

Weka mafuta kijiko kimoja kwenye kikaango na kisha weka soseji zako na uzipike kiasi pande zote kisha epua na weka pembeni.

Weka slesi za mikate kwenye toster na zikiwa tayari unaweza weka siagi ili kuongeza ladha na mvuto.
Andaa mlo wako pamoja na juice, maziwa au chai.

Enjoy!

Mapishi – Saladi ya Matunda


Matunda ni mojawapo wa kundi la vyakula, ni muhimu sana kwa afya bora. Matunda yakitengenezwa vizuri yanavutia sana na yanakuwa ni chakula kizuri sana.

Mahitaji
Embe iliyoiva kiasi
Nanasi
Tango
Tikiti maji
Zabibu
Papai

Matayarisho

1. Ondoa maganda kwenye embe, nanasi, tango, papai na tikiti maji kisha kata kata vipande vidogo vidogo vya mraba

2. Changanya vipande vya matunda kwenye bakuli safikisha weka na zabibu zilizotolewa kwenye kikonyo chake.

3. Weka kwenye friji yapate ubaridi kidogo

4. Saladi yako tayari kwa kuliwa

Waweza kula saladi hii kama mlo wa kati au kama mlo kamili wa usiku.

Enjoy!

Mapishi – Kisamvu cha Karanga


Mapishi yetu leo ni kisamvu cha kuchanganya na karanga. Karibu.

Mahitaji
Majani ya kisamvu
Karanga nusu kikombe
kitunguu kimoja
nyanya mbili
karoti moja
mafuta na chumvi kiasi

Matayarisho

1. Osha kisamvu chako vizuri kisha katakata vipande vidogo vidogo

2. Unaweza kutwanga kwa kutumia kinu au kuchemsha kidogo na kisha kusaga kwa kutumia mashine. Ukitumia mashine uwe makini usije ukasaga sana ukaharibu.

3. Kaanga karanga kidogo na kisha zisage ziwe unga unga.

4. Chemsha kisamvu chako hadi kiive.

5. Katakata kitunguu, karoti na na nyanya

6. Anza kuunga kisamvu kwa kukaanga vitunguu, weka karoti na kisha nyanya na vikishaiva weka kisamvu na koroga pamoja kisha weka karanga. Acha vichemke kwa muda na unaweza pia weka na nazi tui la kwanza.

7. Baada ya muda mfupi epua na kitakiwa tayari. Waweza kula kwa ugali, wali, chapati, makande n.k

Enjoy.

NB: Kumbuka kubakiza kidogo maana kisamvu kikilala kinakuwa kitamu zaidi!

Mapishi – Ndizi Mshare na Nyama


Mapishi yetu ya leo yatakuwa ni ndizi mshare (wengi wanapenda kuziita ndizi moshi) na nyama ya ng’ombe.

Mahitaji
Ndizi Mshare mbichi 16
Nyama ya ng’ombe 1/2 kilo
Vitunguu maji vikubwa 2
Nyanya 1
Pili pili hoho 1
Karoti 1
Mafuta ya kupikia kijiko kikubwa 1
Chumvi kiasi

Matayarisho

1. Osha nyama vizuri na kata kata vipande vidogo unavyopendelea na kisha uichemshe hadi iive. Nyama yenye mafuta kidogo na mifupa kidogo inafaa sana kwa ndizi.

2. Menya ndizi zako vizuri na kuzikata katikati kwa urefu na kisha kwa upana (mshazari), kisha zioshe na kuweka kwenye sufuria yenye maji masafi.

3. Katakata vitunguu, nyaya, karoti na pilipili hoho.

4. Chukua sufuria yako ya kupikia weka ndizi kiasi kisha weka nyama na supu yake, na vitu vyote ulivyokatakata weka pamoja (vitunguu, nyanya, hoho na karoti) kisha weka na ndizi zilizobaki kwa juu. Hakikisha supu inatosha kuivisha ndizi, kama ni kidogo sana ongeza maji ya moto kidogo. Hakikisha ndizi hazizami zote kwenye supu.

5. Bandika jikoni kwa moto wa kiasi na zikichemka, geuza na kisha weka mafuta ya kupikia (na nazi tui la kwanza ukipenda). Acha zichemke hadi ziive kabisa bila kuwa na kiini katikati.

6. Epua na andaa meza tayari kwa kula.

Enjoy!

Mapishi – Kababu (Meat Ball)


Mahitaji
Nyama ya kusaga 1/2kg
Yai 1
Kitunguu maji 1
Kitunguu saumu kilichosagwa kijiko 1
Pilipili manga kijiko cha chai
Chenga za mkata (bread crumbs) kikombe cha chai
Kotmir majani 3
Chumvi kiasi
Mafuta ya kupikia

Matayarisho

1. Katakata vitunguu maji vipande vidogo vidogo, kisha changanya nyama ya kusaga, vitunguu maji ,kotmiri iliyokatwakatwa, vitunguu saum (tangawizi ukipenda), na chenga za mkate.(Ukitumia chenga za mkate halisi ni nzuri zaidi kuliko zile spesho za madukani). Weka chumvi na pilipili manga. Waweza pia weka pilipili mbuzi kama utapendelea.

2. Pigapiga yai na kisha uchanganye kwenye mchanganyiko wako, hakikisha vimechanganyika kabisa. Kisha tengeneza madoge madogo ya mviringo na weka pembeni. Hakikisha madonge sio makubwa sana ili nyama iweze iva vizuri.

3. Weka kikaango jikoni na mafuta na kiasi ili madonge yako yasizame, weka kababu zako kwenye mafuta na ziache ziive upande mmoja kisha geuza na upande mwingine. Zingatia moto uwe wa kiasi ili zisibabuke bali ziive hadi ndani kabisa.

4. Epua na weka kwenye sinia yenye karatasi za jikoni ili zichuje mafuta yote kisha weka mezani tayari kwa kula.

Waweza kula na chai, juis, soda au hata mchuzi wa maharage, mboga za majani n.k jinsi upendavyo mwenyewe.

Enjoy!

Bajia za Dengu


Kuna msomaji ameomba mapishi ya bajia hivyo leo tutaangalia mapishi ya bajia za dengu.

Mahitaji
Unga wa dengu kikombe kimoja
Vitunguu maji 2 (Katakata vipande vidogo vidogo)
Vitunguu saumu vilivyo sagwa kijiko cha chai 1
Baking Powder kijiko cha chai 1
Maji Kiasi
Chumvi
Mafuta ya kukaangia
Pilipili , Kotmiri ukipenda

Matayarisho



1. Kwenye bakuli kubwa changanya unga wa dengu na vitunguu maji na vikisha changanyika weka vitunguu saumu, kotmiri iliyokatwa katwa na baking powder. Weka chumvi kiasi kidogo.

2. Weka maji kidogo kidogo hadi mchanganyiko wako uwe mzito kisha uache kwa muda.

3. Bandika kikaango jikoni na weka mafuta, yakishachemka chota mchanganyiko wako kwa kijiko na kuweka kwenye mafuta. Angalia usiweke mara nyingi sana ili bagia zisijeshikana.

4. Zikiiva na kuanza kubadilika rangi epua na uweke mahali zitoke mafuta. Hakikisha moto sio mkali sana ili ziive na sio kubabuka.

5. Andaa tayari kwa kula na kinywaji chochote.

Enjoy!

Mapishi – King Fish wa Kukaanga


Mahitaji
1. Samaki aina ya kingfish
2. Unga wa ngano 1/4kg
3. Chumvi
4. Mafuta ya kupikia

Matayarisho
1. Safisha samaki na kata kata vipande vidogo kwa kadiri unavyopendelea.
2. Weka chumvi kwenye kila kipande kisha unyunyuzie unga wa ngano kukifunika kabisa. Fanya hivyo kwa vipande vyote.
3. Weka mafuta kwenye kikaango na yakisha chemka weka samaki wako. Acha upande mmoja uive na geuza upande mwingine.
4. Epua tayari kwa kula.

Unaweza kula wakiwa wamekaangwa tu au unaweza kuunga kwa nazi baada ya kumaliza kukaanga. Uchaguzi ni wako.
Enjoy!

Mapishi – Mchemsho wa Samaki


Leo jikoni tunaangalia mapishi ya mchemsho wa samaki. Mchemsho huu ni kwa ajili ya watu wawili.

Mahitaji
. Samaki wakubwa kiasi 2 (Hapa natumia changu)
. Viazi mviringo 5
. Bamia, karoti, pilipili hoho na kitunguu maji
. Tangawizi
. Ndimu 2
. Chumvi

Matayarisho
1. Andaa samaki na kisha ukamulie ndimu moja.
2. Menya viazi na ukate vipande vinne kila kiazi.
3. Katakata bamia, karoti, kitunguu na pilipilh hoho.
4. Menya tangawizi na uitwange.
5. Bandika viazi na maji kiasi kisha weka chumvi na vitunguu.
6. Vikianza kuiva weka tangawizi, hoho, karoti, bamia na samaki. Hakikisha kuna supu ya kutosha ila isiwe nyingi sana.
7. Acha vichemke kwa dakika kumi hadi 15 kisha epua.

Andaa mezani ukiweka kipande cha ndimu, nyanya na tango.

Enjoy!